Majukumu ya Jeshi la Kujenga Taifa
MAJUKUMU YA MSINGI (Objectives)
1. Malezi ya Vijana
- Vijana kufundishwa moyo wa kupendana bila kujali tofauti za itikadi, dini, kabila na kipato.
- Kupenda kazi za mikono.
- Kuthamini na kuendeleza mila, desturi na kudumisha utamaduni wa Taifa.
- Kuwa raia wema, wanaojiamini, wanaojituma, wenye uzalendo na kuipenda nchi yao.
2. Ulinzi wa Taifa
- Kuwapa vijana mbinu za kijeshi wawe Jeshi la akiba, kuwaandaa vijana watakaofaa kujiunga na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama.
- Kuwaandaa vijana kusaidia katika majanga mbalimbali, mfano mafuriko, moto na ajali mbali mbali.
3. Uzalishaji Mali
- Ili kuwafanya vijana wa kitanzania waepukane na kusumba kuwa kazi za ofisini ndio njia pekee na bora inayomuwezesha mtu kuishi, JKT linahusika na uzalishaji mali kwa lengo la kuwawezesha vijana kujiajiri katika sekta mbali mbali mara baada ya kumaliza mkataba na JKT. Uzalishaji mali unaofanywa na JKT ni pamoja na:-
- Kujenga na kukarabati majengo
- Viwanda na Kilimo
- Madini na Nishati
- Utalii
- Ulinzi kwa Taasisi binafsi (Security Guard Services)
- Maduka (Super Market)
- Kuunganisha magari na mitambo
- Huduma za elimu
Mpango Mkakati wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi
Jeshi la Kujenga Taifa limekuwa likiendesha uzalishaji kupitia kilimo, mifugo na uvuvi vikosini kama mashamba na miradi darasa kwa ajili ya mafunzo ya stadi za kazi kwa Vijana.
Idadi ya Vijana imekuwa ikiongezeka na kusababisha wengi kutaka kujiunga. Ongezeko hilo limeongeza mahitaji ya kuzalisha chakula kimkakati kwa matumizi ya Vijana, biashara na uhakika wa chakula nchini.
Mwaka 2019 JKT ilibuni na kuunda kamati chini ya Brigedia Jenerali Hassan Mabena wakati huo akiwa na cheo cha Kanali, iliyoanzisha mpango mkakati wa mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi. Kamati hiyo ilifanya yafuatayo:
- Kupitia takwimu za uzalishaji vikosini na kuchagua maeneo na mazao mkakati ya kusaidia kufikia malengo ya kujitosheleza kwa chakula.
- Kuandaa andiko la kilimo, mifugo na uvuvi mkakati.
- Kusimamia upimaji mashamba ya kimkakati kwa ‘GPS’ ili kufahamu ukubwa halisi wa mashamba hayo.
- Kuzingatia matumizi ya teknolojia kwenye uzalishaji ikiwemo upimaji wa afya ya udongo, matumizi sahihi ya kanuni za sayansi ya uchumi wa kilimo, zana bora za kilimo, umwagiliaji na kuchakata mazao kibiashara.
- Kusimamia uzalishaji wa tija vikosini, ili kufikia na kuvuka malengo yaliyowekwa kimkakati.
Malengo ya Mkakati
Mkakati huo ulizingatia uchambuzi na mahitaji ya hali halisi ulikuwa na malengo yafuatayo:
- Kuongeza uzalishaji wa mazao kwa tija na kujenga uwezo wa kujitosheleza kwa chakula.
- Kuwapatia Vijana mafunzo ya stadi za kazi na kuwajengea uwezo wa kujiajiri kupitia teknolojia mpya za uzalishaji.
- Uzalishaji wa mbegu bora ili kuongeza uhakika wa chakula nchini.
- Kuchangia uchumi wa viwanda kupitia shughuli za uzalishadi zitakazofanywa na JKT.
- Ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na barabara.
- Ujenzi wa maghala.
- Ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao.
- Utoaji mafunzo kupitia mpango mkakati.
Mafanikio ya Mpango Mkakati
Uanzishaji na utekelezaji wa mpango mkakati wa kilimo, mifugo na uvuvi, umeleta mafanikio makubwa hasa katika kuongeza ufanisi kwenye utekelezaji wa majukumu ya JKT. Mpango huo umefanikiwa katika mambo yafuatayo:
- Ujenzi wa skimu ya umwagiliaji Chita JKT yenye uwezo wa kumwagilia takribani ekari 12,000 za mpunga na mahindi.
- Uanzishaji shamba kubwa na la kisasa la ufugaji samaki kwa njia ya matangi na uzalishaji wa vifaranga vya samaki Chita JKT.
- Kuongeza uzalishadi wa zao la mpunga Chita JKT.
- Kuongeza uzalishaji wa mahindi katika Vikosi vinavyolima zao hilo kwa tija.
- Ununuzi wa zana za kisasa za kilimo. Mfano; matrekta, harrow, rotter vetter, planter, combine harvester, n.k
- Ujenzi wa maghala makubwa ya mazao katika Vikosi vya kilimo mkakati.
- Vijana kupata elimu ya kilimo cha kisasa na jinsi ya kutumia na kuifanyia matengenezo mitambo ya kilimo.
- Kuongeza ushirikiano baini ya JKT na taasisi zingine za kiserikali ikiwamo SUA, TARI kwenye utafiti wa mbegu.
SHIRIKA LA UZALISHAJI MALI LA JESHI LA KUJENGA TAIFA
Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT) ni tawi la kiuchumi linalojishughulisha na uzalishaji mali kibiashara, ili kusaidi kupunguza gharama kwa Serikali katika kuendesha JKT.
SUMAJKT ilianzishwa Julai mosi, 1981 kwa Sheria ya Uanzishwaji Mashirika ya Kibiashara katika Taasisi za Umma (The Corporation Sole (Establishment) Act, No. 23 of 1974 Cap 119 RE 2002).
Shirika linazalisha mali kupitia sekta za ujenzi, kilimo, mifugo na uvuvi, huduma na biashara na viwanda. Linaendelea kuboresha miradi na kampuni zake, pia kuanzisha miradi mipya ili kuongeza mapato na kutekeleza majukumu yake.
Chimbuko la SUMAJKT
SUMAJKT ilianzishwa kutokana na wazo la Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alitoa wazo hilo mwanzoni mwa miaka ya sabini alipotembelea Kambi za JKT kujionea shughuli za mafunzo, malezi ya Vijana na uzalishaji mali. Moja ya Kambi alizotembelea ni Ruvu wakati huo, kambi nyingi za JKT zilikuwa zikiathiriwa na uhaba au ucheleweshaji fedha za kujiendesha, hali iliyosababisha kutofikia malengo ya kuanzishwa kwao.
Ili kutatua tatizo hilo, Mwalimu Nyerere aliona umuhimu wa uzalishaji mali ndani ya JKT kuendeshwa kibiashara, hivyo aliagiza Wizara ya Ulinzi na JKT kulifanyia kazi wazo hilo. Hii ilisababisha kuundwa Tume kuangalia jinsi mashirika na taasisi zingine za umma zinavyoendeshwa uzalishaji mali kibiashara.
Machi 1981. Mawaziri walijadili Waraka wa Baraza la Mawaziri Namba 25 wa mwaka 1980 uliotayarishwa na Wizara ya Ulinzi na JKT, kuhusu kuundwa kwa Shirika la Kiuchumi. Baada ya kuujadili, Rais alikubaliana na mapendekezo ya kuanzishwa Shirika la Uzalishaji Mali ndani ya JKT.
Baadhi ya majukumu yaliyoelekezwa SUMAJKT yalikuwa ni kufuatilia miradi ya uzalishaji mali iliyokuwa ikitegemea fedha kutoka serikalini, kupitia Bajeti ya Serikali, kuliwezesha Shirika kuwa na uwezo mkubwa kifedha wa kukopa na kukopesha, kuiongeza fedha za mitaji miradi iliyoonekana kuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi, kuwezesha Shirika kuzalisha mali, kuuza na kutoa huduma kibiashara.
Shirika lilitakiwa kufanya Upembuzi yakinifu wa miradi ya uzalishaji mali iliyokuwa ikiendeshwa katika Kambi za JKT kabla ya kuichukua na kuuingiza kwake.
Upembuzi yakinifu ulitakiwa ufanywe kabla ya kuanzisha miradi mipya. Baada ya upembuzi huo kuonesha kuwa mradi uliolengwa unaweza kuleta faida, jukumu la Shirika lilikuwa kutoa mtaji au mkopo wa kuendesha mradi husika, kununua zana, pembejeo, kuongeza utaalamu wa uzalishaji na kutafuta masoko.
Kifungu cha 3(1) cha sheria iliyoanzisha Shirika, ilimpa Rais mamlaka ya kutoa amri ya kuundwa Shirika la kibiashara katika taasisi za umma.
Shirika lilianzishwa rasmi kupitia Tangazo la Serikali Namba 94 la Julai mosi, 1981 na kuitwa SHIRIKA LA MKUU WA JKT. Tangazo hilo lilitoa orodha ya sekta za uzalishaji mali zitakazosimamiwa na Shirika, ingawa halikueleza madaraka ya Mkuu wa JKT katika muundo wake.
Tangazo hilo lilifutwa, badala yake Amri ya Rais kupitia Tangazo lingine Namba 116 la Septemba 24, 1982 lilichukua nafasi yake. Pamoja na kutaka sekta za uzalishaji mali zitakazosimamiwa na Shirika lilieleza kuwa Mkuu wa JKT atakuwa ndiye Afisa Mtendaji Mkuu wake.
Shirika lilianza na vitengo tisa vyenye miradi 25. Ilipofika mwaka 1983 vitengo vingine saba vyenye miradi 14 viliongezwa, hivyo kuwa 16 vyenye miradi 39. Makamanda Vikosi walikuwa mameneja wa miradi iliyokuwa inaendeshwa katika kambi za JKT.
Mwaka 1985, Waziri wa Ulinzi na JKT alitoa mwongozo namba moja ukielekeza jina, anwani, nembo, muundo, watendaji na sifa wanazostahili kuwa nazo. Pia, ulifuta waraka na miongozo mingine ya awali ya uendeshaji Shirika. Kuanzia mwaka huo, jina la Shirika lilibadilishwa na kuwa Shirika la Uzalishaji Mali la JKT badala ya Shirika la Mkuu wa JKT. Waziri wa Ulinzi na JKT alitoa miongozo mingine miwili; Namba 2/2003 na 3/2008.
Tangazo la Serikali Namba 116 la Septemba 24, 1982 lilifutwa, badala yake Amri ya Rais kupitia Tangazo la Serikali Namba 326 la Septemba 18, 2009 lilichukua nafasi yake. Tangazo hili liliongeza wigo wa uzalishaji mali wa Shirika kwenye biashara ya nishati na madini, utalii, ulinzi binafsi, maduka makubwa, usindikaji matunda, uundaji mitambo na magari, huduma za elimu, biashara za magari, mashamba ya kilimo na mifugo na shughuli zingine zenye faida kwa Shirika.
Kazi za SUMAJKT
Shirika la Uzalishaji mali la Jeshi la Kujenga Taifa, linatekeleza majukumu mbalimbali yakiwemo Uvuvi, Kilimo, Ufugaji, Viwanda, Biashara na Huduma. Aidha katika kutekeleza majukumu hayo, SUMAJKT limeanzisha kampuni mbalimbali kama ifuatavyo:-
- SUMAJKT Construction Co. Ltd
- Agri-Business Co. Ltd
- Meat Supply Project
- Bottling Co. Ltd
- Garments Co. Ltd
- Chang’ombe Furniture Co. Ltd
- Shoe and Leather Products Co Ltd
- Mlale Milling Co. Ltd
- Guard Ltd
- Auction Mart Co. Ltd
- Cleaning and Fumigation Co. Ltd
- Catering and Services Co. Ltd
- Insurance Broker Co. Ltd
- Port and Services Co. Ltd
- Logistics Co. Ltd
- Pharmaceutical Co. Ltd,
- Agri-Machinery Project, Energy na Clearing and Forwarding Agency.